Muktasari:
- Baada ya Mwananchi kumuibua mgonjwa aliyekaa hospitali kwa zaidi ya miaka 16, Paulo Matemu (48), mkazi wa Kirua Vunjo Watanzania waanza kumchangia.
Moshi. Zikiwa zimepita siku 11 tangu Gazeti la Mwananchi liandike habari ya mgonjwa aliyekaa hospitali kwa miaka 16, Paulo Matemu (48), mkazi wa Kirua Vunjo, Wilaya ya Moshi, Mkoa wa Kilimanjaro wadau mbalimbali wameguswa na maisha yake na kuanza kumchangia kiasi cha Sh600,000.
Matemu ambaye kwasasa anajisaidia kupitia ubavuni, baada ya kupata ajali ya kuanguka kutoka ghorofa ya tatu alikokuwa akifanya kazi ya ujenzi mwaka 2007 na kumsababishia kuumia uti wa mgongo uliompelekea kupooza miguu amelazwa katika Hospitali ya Kilema, iliyopo Marangu akiendelea na matibabu.
Mpaka sasa Matemu amefikisha miaka 16 akiwa hospitali akiendelea na matibabu huku wazazi wake wote wawili pamoja na ndugu zake wengine sita wakiwa wameshafariki dunia akiwa bado hospitalini akipigania uhai wake ambapo hakuweza kushiriki mazishi ya ndugu zake hao.
RELATED
- Simulizi ya aliyekaa hospitali miaka 16 akitibiwaKitaifa Nov 06
- VIDEO: Miaka 14 hospitali akipigania uhai wakeKitaifa Nov 07, 2020
Hata hivyo Matemu alisema baada ya kupata ajali, alitibiwa katika hospitali mbalimbali ikiwemo ya Mount Meru iliyopo Arusha, KCMC na baadaye hospitali ya Kilema ambako anaendelea kutibiwa na kupatiwa mahitaji mengine.
Novemba 5, mwaka huu, Mwandishi wa Gazeti hili alipofanya mahojiano na mgonjwa huyo akiwa hospitalini hapo, alieleza kwa machungu namna ambavyo anatamani kurejea nyumbani kwao ikiwa hana ndugu lakini na nyumba ya udongo aliyokuwa akiishi alielezwa kuwa imeshabomoka.
Aliwaomba Watanzania na serikali kuona namna ya kumsaidia ili aweze kupata msaada wa fedha za kuweza kumjengea nyumba angalau hata vyumba viwili ili aweze kurejea nyumbani pindi atakapopata nafuu.
Matemu amelishukuru Gazeti la Mwananchi kwa kumuibua na kusema limekuwa ni msaada mkubwa kwake kwa namna ambavyo walimuibua na sasa anaona Watanzania wakiungana na yeye katika changamoto anazopitia.
Kwa machungu alieleza huku akiwa amekaa kwenye kiti mwendo (wheel chair) “Wazazi wangu na ndugu zangu wengine sita wote wameshafariki, walifariki wakati nipo hospitali nimelazwa. Nawaza nikitoka hospitali kurudi nyumbani, sijui nitapakuta vipi maana hata mke wangu alinikimbia na kuniachia mtoto wa miaka sita baada ya kupata ajali hiiā¦
Nimekuwa mlemavu, sina ndugu, karibu wote wamekufa, nyumba zilizoachwa na wazazi wangu ambazo ningeweza kukaa, nazo zimeanguka, kwasababu zilijengwa kwa udongo.”
Hayo ni baadhi ya maneno aliyokuwa akiyatamka Matemu wakati akizungumzia hali yake na changamoto ya maisha aliyokutana nayo baada ya kupata ajali.
Akiwashukuru Watanzania ambao wameguswa na maisha yake, amesema mpaka sasa ameshapokea Sh600,000 kutoka kwa watu mbalimbali ambao wameendelea kumtumia kwenye mitandao yake ya simu.
“Nawashukuru Watanzania wenzangu kwa namna ambavyo mmeguswa na changamoto hii ya maisha iliyonikuta na ni maisha ambayo yeyote anaweza kuyapitia. Niwaombe msikate tamaa kunisaidia, mimi ni Mtanzania mwenzenu naomba msaada wenu, nipate chochote kile niweze kupata angalau vyumba viwili pale nyumbani maana nyumba iliyokuwepo ya udongo ilianguka,” amesema
“Natamani kwa maisha haya na muda ambao nimebakiza hapa duniani, kwa upendo wenu muweze kuwa faraja kwangu maana sina wakumweleza changamoto zangu zaidi yenu, nyie ndio ndugu zangu mliobaki kunisaidia.”
Atakaye guswa kumsaidia Matemu namba zake za simu ni; 0679828334 na 0710858334.