Ijumaa, Novemba 17, 2023
Mwandishi mwandamizi
Mwananchi Communications Ltd (MCL)
Dar es Salaam. Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam imemhukumu Wibati Komba kifungo cha miaka mitano jela, baada ya kukiri kosa la kumuua mpenzi wake bila kukusudia, baada ya kumshuku alitoka kuchepuka.
Kilichomfanya amhisi hivyo ni manii alizozikuta kwa mpenzi wake huyo alipotaka kumwingilia kimwili wakiwa sebuleni katika nyumba waliyokuwa wakiishi.
Hii ilimfanya apandwe na hasira na kuamua kumnyonga shingo kwa kutumia kipande cha nguo hadi kumuua, akaupeleka mwili chumbani na kuufunika kwa shuka kisha kuuburuta hadi kibanda cha mifugo na kuutelekeza.
Katika uamuzi wake, Jaji Abdalah Gonzi alisema kosa la mauaji ya bila kukusudia linaangukia kifungu cha 198 cha Kanuni ya adhabu ambacho kinatoa adhabu hadi ya kifungo cha maisha kwa anayepatikana na hatia ya kosa hilo.
“Hii ina maana Mahakama ndio yenye uamuzi kutoa adhabu yoyote ambayo haizidi kifungo cha maisha. Hakuna kiwango cha chini cha adhabu, lakini sheria imeweka tu kiwango cha juu cha adhabu kuwa kifungo cha maisha,” alisema.
Jaji alisema wakili wa Serikali, Doroth Massawe aliiomba Mahakama kutoa adhabu kali, ili kutoa fundisho kwa mshtakiwa kutorudia kosa kama hilo na kutuma pia ujumbe kwa jamii kutofanya kosa la jinai linalofanana na hilo.
Hata hivyo, alisema adhabu kali inatakiwa kutolewa kwa mtu anayerudia kutenda kosa ili kama alipewa adhabu ndogo, basi adhabu kali inatakiwa ijaribiwe ili asirudie kosa hilo.
“Kama mwaka mmoja aliokaa mahabusu haukumpa funzo, basi miaka miwili lazima ijaribiwe na kuendelea, lakini kwa mshtakiwa aliyepo mbele yangu wakili wa Serikali alipoulizwa alisema hana kumbukumbu za nyuma za makosa,” alisema.
Kulingana na Jaji, anatoa adhabu kwa mshtakiwa ili kumuonyesha alichokifanya kilikuwa kibaya na kwamba kulikuwa na njia za kibinadamu kutatua mgogoro wa kimapenzi kuliko za kumuua mpenzi wake.
Jaji alisema ametilia maanani kuwa mshtakiwa alijisalimisha polisi ili kutoa nafasi kwa vyombo vya dola kufanya kazi yake na alikuwa tayari kukiri kosa lake katika maelezo yake ya onyo aliyoandika polisi na pia kwa mlinzi wa amani.
Hivyo, Jaji akamhukumu kifungo cha miaka mitano, lakini kutokana na ukweli ameshakaa mahabusu mwaka mmoja na miezi minne, muda huo ukapunguzwa hivyo mshtakiwa atatumikia kifungo cha miaka mitatu na miezi sita jela.
Tukio la mauaji lilivyokuwa
Novemba 2, mwaka huu mshtakiwa huyo alifikishwa mahakamani akikabiliwa na kosa la mauaji ya bila kukusudia kwamba Aprili 25, 2022, eneo la Chamazi Wilaya ya Temeke, Dar es Salaaam alimuua Magret Kimbulu.
Baada ya kusomewa shtaka hilo mbele ya wakili wake, Agatha Fabian, alikiri na ndipo upande wa mashtaka ukiongozwa na wakili Doroth aliiomba Mahakama amsomee maelezo ya namna alivyotenda kosa.
Ilielezwa Aprili 25, 2022 mshtakiwa na marehemu walikuwa na safari ya kwenda Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), na siku hiyo marehemu alikuwa amefungasha nguo zake kwa kuwa mshtakiwa alikuwa hamhitaji arudi kwake.
Wakiwa njiani, waligombana kwani mshtakiwa alimshuku alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na wanaume wengine, hivyo kila mmoja alikwenda na njia yake lakini jioni walikutana, marehemu akaomba msamaha.
Mshtakiwa alikubali na kumsamehe na walirudi wote nyumbani kwa mshtakiwa na walipofika baada ya kitambo kidogo mshtakiwa aliondoka nyumbani, lakini huku nyuma marehemu naye aliondoka nyumbani.
Kulingana na maelezo hayo, saa 12 jioni ya siku hiyo, mshtakiwa alirudi nyumbani na kumkuta marehemu naye akiwa amerudi na ndipo alimshuku alikuwa hajaacha tabia za mahusiano na wanaume wengine.
Hata hivyo, jioni hiyo walikula chakula pamoja, ingawa marehemu hakuonyesha nidhamu wakati wa kula, hivyo kutokana na vitabia hivyo, mshtakiwa hakumaliza chakula, akaamua kwenda sebuleni kupumzika.
Baada ya chakula hicho, marehemu alianza kucheza muziki uliokuwa ukitokea kwenye redio, mshtakiwa akamshika mpenzi wake na kubaini hakuwa amevaa chupi, akapata mshawasha wa kumuingilia kimwili hapo sebuleni.
Katikati ya kitendo hicho, mshtakiwa alibaini marehemu alikuwa na manii (mbegu za kiume) sehemu zake za siri na hiyo ikamfanya ashuku kuwa atakuwa ameingiliwa kimwili na mwanamume mwingine kabla yake.
Hiyo ilimuudhi mshtakiwa na ndipo alipoamua kumuua ambapo alimkamata na kumnyonga kwa kutumia nguo na kutelekeza mwili kwenye banda la mifugo na kutoroka hadi Aprili 29, 2023 alipojisalimisha mwenyewe polisi na kukiri kosa.